Baraza la Kitaifa la Ushauri la Waislamu nchini Kenya limekemea vikali makabiliano ya hivi karibuni kati ya kikosi cha usalama cha kaunti na vijana waliokuwa wakiandamana nje ya Bunge la Kaunti ya Mombasa.
Akizungumza na wanahabari, Rais wa baraza hilo, Sheikh Juma Ngao, alikosoa mashirika ya kiraia yaliyohusika katika kuandaa maandamano hayo, akisema malalamishi yanapaswa kuwasilishwa kupitia njia halali na zinazotambuliwa na Katiba.
“Mombasa ni jiji la kitalii, na usalama unapaswa kuwa kipaumbele cha kila mtu anayejali jiji letu,” alisema Sheikh Ngao.
Alidai kuwa baadhi ya wanaharakati wa haki za binadamu wamekuwa wakitumia makabiliano badala ya njia za kisheria, hali ambayo alisema inaweza kuhatarisha usalama na utulivu wa Mombasa.
Ngao alizitaka taasisi za kiraia kutumia njia zinazotambuliwa kisheria kuwasilisha malalamishi yao, ikiwemo kupitia Bunge la Kaunti, Seneti na ofisi nyingine za umma katika serikali za kaunti na kitaifa.
Kauli hiyo iliungwa mkono na naibu wake, Abubakar Amin, ambaye alitoa wito wa utulivu na mazungumzo ya amani katika kushughulikia masuala yanayowahusu wananchi.
Baraza hilo pia lilieleza wasiwasi kuhusu mipango ya kufunga baadhi ya mashirika ya serikali, likisema hatua hiyo inaweza kudhoofisha taasisi zinazotekeleza majukumu muhimu katika kukidhi mahitaji ya jamii za Pwani.
Sheikh Ngao alikosoa zaidi pendekezo la kufungwa kwa Mamlaka ya Maendeleo ya Pwani (CDA), akisema taasisi hiyo imekuwa ikichangia katika miradi mbalimbali ya kiuchumi na maendeleo katika eneo la Pwani.
Baraza hilo limeeleza kuwa kufungwa kwa CDA kutawaathiri wananchi wanaonufaika na programu zake, na limeipa serikali siku 14 kutafakari upya uamuzi huo. Vinginevyo, limesema litachukua hatua za kisheria kulinda mamlaka hiyo.
Ngao pia alitaka serikali kufanya ushirikishwaji wa maana wa umma kabla ya kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu mustakabali wa CDA, akisisitiza kuwa jamii zinazonufaika moja kwa moja na programu za mamlaka hiyo zinapaswa kupewa taarifa na kushauriwa ipasavyo.

Comments
Post a Comment